Benki ya CRDB inajivunia kutunukiwa tuzo ya Benki Bora nchini kwa mwaka 2022 na Jarida la Euromoney.
Ikiwa ni tuzo yake ya pili kuinyakua, baada ya kushinda tuzo kama hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2004, ushindi huo haukuwa wa kubahatisha bali jitihada na mikakati ya benki hiyo.
Furaha isiyo kifani imemsogeza karibu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela ambaye anakiri kuwa, “Tuzo ya Euromoney inathibitisha nafasi ya CRDB kama benki inayoongoza nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akitoa hotuba yake wakati wa kupokea tuzo ya Euromoney kama Benki Bora Tanzania.
Pia inatambua mafanikio ya mageuzi ambayo yamesababisha ukuaji endelevu wa benki yetu na kunufaisha wateja wetu, wawekezaji na uchumi wa nchi kwa ujumla,” Nsekela aliongeza.
Anasema kuwa mafanikio hayo ya katikati ya mwaka yanaakisi mwenendo mzuri wa benki uliowezesha ukuaji endelevu wa tarakimu mbili katika kipindi cha miaka minne iliyopita ikichagizwa na mageuzi ya kimkakati na uvumbuzi.
Pia anaelezea kuongezeka kwa kiwango cha faida cha benki hiyo kwa miaka miwili iliyopita ambapo faida baada ya kodi iliongezeka kutoka Sh165.2 bilioni mwaka 2020 hadi kufikia Sh268.2 bilioni mwaka 2021.
Hii ndiyo faida kubwa zaidi katika historia ya benki na hiyo inadhihirisha thamani ya mageuzi endelevu ambayo benki imeyafanya katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Kulingana na Nsekela, vipimo vingine muhimu vilivyoupa ushindi benki hiyo ni uendelevu wa uzalishaji wa thamani kwa wanahisa wake (na washikadau wengine) kupitia mapato endelevu.
Pia imekuwa taasisi inayoongoza kibiashara kusaidia minyororo ya thamani ya kiuchumi inayoendelea kuboresha maisha ya Mtanzania mmoja mmoja na uchumi.
“Katika eneo la ubunifu, benki inaendelea kushika usukani wa soko la Tanzania, ubunifu katika kubadilisha maisha katika sekta ya huduma za fedha katika nyanja ya malipo na bidhaa zilizoboreshwa.
Benki hiyo inaonyesha ukubwa wake wa mizania ya Sh 9.4 trilioni kama kichocheo chake cha kiuchumi mbali na kuwezesha sekta muhimu za uchumi kama vile; kilimo, miundombinu, viwanda na utalii, miongoni mwa mambo mengine.
Mafanikio ya Benki ya CRDB vilevile yanachagizwa na kampuni yake tanzu ya CRDB Burundi ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika biashara yake katika kipindi cha miaka 10 toka kuanzishwa kwake.
“Benki itaendelea kutanua wigo wake na hivi karibuni inatarajia kuingia katika soko la Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) kurahisisha ufanyikaji wa biashara baina ya Tanzania na DRC ukizingatia nchi hiyo inategemea bandari ya Dar es Salaam kwa uuzaji na ununuaji wa bidhaa,” anafafanua zaidi.
Kwa upande mwingine, Nsekela anaeleza kuwa Benki ya CRDB ni benki ya kwanza ya biashara Afrika Mashariki iliyoidhinishwa na Mfuko wa Hali ya Hewa ya Kijani (GCF) kama taasisi mwezeshaji wa uboreshaji wa mazingira nchini.
Credit Mwananchi